Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, nchini Lebanon kuliandaliwa hafla kubwa na ya kina iliyowakutanisha wanazuoni wa dini kutoka madhehebu na makundi mbalimbali kwa ajili ya kumuenzi na kutoa taazia kufuatia kufariki kishahidi Ayatullah al-Udhma Imam Sayyid Ali Khamenei (qs). Katika hafla hiyo, wahadhiri mbalimbali walizungumzia njia ya kijihadi na ya kielimu ya Imam huyo, nafasi yake, misimamo yake mashuhuri, pamoja na athari zake kubwa katika eneo la Mashariki ya Kati na ulimwengu wa Kiislamu.
Sheikh Ali al-Khatib, Naibu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia nchini Lebanon, alisema katika hotuba yake kuwa; Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya kuuawa kishahidi Imam Sayyid Ali Khamenei, "si ile ile kama ilivyokuwa zamani," akisisitiza kuwa leo nchi hiyo ipo katika mwanzo mpya na hatua mpya ya nguvu.
Aliongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa sasa inaandika mwanzo mpya katika ulimwengu mzima kwa namna ya kukabiliana na Magharibi na changamoto zake, huku akiuelezea ulimwengu wa sasa kuwa ni ulimwengu "usiotambua maadili na uliojengwa juu ya misingi dhaifu."
Sheikh al-Khatib aliendelea kusema kuwa; Marekani na uongozi wake wanaishi kwa misingi ya uongo na unafiki pekee, na kwamba chombo wanachokitumia kuufanya ulimwengu uwatii ni nguvu na mabavu.
Naibu Mwenyekiti huyo wa Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia alisisitiza kuwa; mizizi ya fikra, dini na maadili ya uongozi wa Iran imejikita kwa kina miongoni mwa wananchi wa Iran, mataifa ya Kiarabu, Umma wa Kiislamu na mataifa yote huru duniani.
Aidha alisema: "Kwa mtazamo wangu, kupotea kwa kiongozi huyu mkubwa kumeambatana na mafanikio makubwa; sisi tumepata dini yetu, maadili yetu na mustakabali mpya kwa ajili ya Umma wetu, na hivi karibuni tutashuhudia matunda yake."
Sheikh Ali al-Khatib pia alisisitiza kuwa, leo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesimama kukabiliana na dola kubwa zaidi na kiburi duniani. Akiwakosoa wale walioweka matumaini yao katika chaguzi potofu na kuuza nchi yao, wananchi wao na damu za mashahidi, alisema: "Watu hao hawana thamani yoyote hata mbele ya mabwana wao."
Kwa upande mwingine, Sheikh Zuhair Ju'eid, Naibu Mwenyekiti wa Muungano wa Wanazuoni wa Kiislamu wa Lebanon, alisisitiza msimamo wake wa kupinga mfumo wowote wa mazungumzo kati ya serikali ya Lebanon na utawala wa Kizayuni, akieleza wazi kwamba Marekani si mpatanishi, bali ni "mshirika kamili katika kumwaga damu yetu."
Sheikh Ju'eid pia alisisitiza kushikamana na njia ya "Islamabad" kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Marekani, na kusema: "Hatutarudi nyuma katika kulinda mamlaka ya Lebanon, wala hatutakubali kuacha hata chembe ya ardhi ya nchi hii."
Katika mwendelezo wa hafla hiyo, Askofu Ibrahim Shaheen, Mkuu wa Mahakama ya Kiroho ya Kanisa la Orthodox mjini Tripoli, alitoa hotuba iliyolaani vikali mauaji ya Imam Sayyid Ali Khamenei (qs).
Vilevile, Sayyid Ali Hijazi, akiwakilisha Hawza, alihutubia hafla hiyo na kusisitiza fadhila za Imam Shahidi Khamenei (qs), huku akieleza nafasi yake kubwa ambayo kheri na baraka zake zimeenea katika eneo zima na ulimwengu wa Kiislamu.
Maoni yako